Ijumaa 11 Septemba 2026 - 21:11
Muungano wa Wanamapinduzi wa Bahrain Watahadharisha Kuhusu Kunyimwa Haki Mashia

Hawzah/ Muungano wa Mapinduzi ya Februari 14 wa Bahrain umetangaza katika taarifa yake kwamba: Wananchi wa Bahrain hawatakubali mpango wa mauaji ya kimbari na kuhalalisha uhusiano na Israel, na wataendelea kupinga hukumu za kuwakandamiza kidini na kutotii hukumu hizo.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Baraza la Kisiasa la “Muungano wa Vijana wa Mapinduzi ya Februari 14 wa Bahrain”, limewapongeza wanafunzi na wasomi kwa kuanza mwaka mpya wa masomo nchini Bahrain na kuingia katika msimu mpya wa maisha yao ya kielimu na kitaaluma.

Baraza hilo, katika taarifa yake ya kila wiki iliyochapishwa kupitia tovuti ya Muungano huo, limewataka wanafunzi kutoa juhudi zao zote katika kutumia muda vizuri kwa ajili ya kujipatia elimu na kufikia viwango vya juu zaidi; jambo ambalo linatokana na msingi wa uhusiano wao wa kidini na kitaifa, bali pia ni ulazima mkubwa kwa ajili ya kuhifadhi utambulisho wao na kuimarisha nguvu ya wananchi katika mazingira ya changamoto wanazokabiliana nazo, ambazo zinalenga kudhoofisha uwepo wao wa kistaarabu na kiroho.

Baraza hilo pia limewataka walezi na wazazi kufuatilia hali za watoto wao licha ya vikwazo na kulengwa kwao, kuwaandalia mazingira yanayofaa, na kuweka mkazo katika kuhakikisha wanapata malezi bora ya kielimu na kidini kupitia elimu ya dini inayohifadhi utambulisho wao halisi na uhusiano wao wa kimsingi, na kuwalinda dhidi ya athari za mpango hatari unaotishia maadili na tabia zao njema.

Muungano wa Wanamapinduzi wa Bahrain umelaani sharti la Wizara ya Sheria linalowataka wahubiri kupata kibali cha kiusalama kabla ya kushiriki katika mimbari za mihadhara na shughuli za mawaidha na kaswida za kidini katika misikiti na Husainiya, ukisema: Hatua hii haikuwa ya kushangaza; kwa sababu familia ya Al Khalifa imetangaza mara nyingi nia yake ya wazi ya kuwachukia Mashia na kutosita kupambana na utambulisho wao, viongozi wao, taasisi zao na Hawzah zao za kielimu. Kwa miaka mingi, “Firauni Hamad” ametoa mwanga wa kijani kwa kutolewa mfululizo kwa maamuzi na hukumu mbalimbali za kuwazunguka Mashia kwa vikwazo na kuifanya imani na ibada zao kuwa makosa ya kisheria; kuanzia suala la hali ya mtu binafsi, kuhalalishwa kisheria Khums na misafara ya maombolezo, hadi kuvunjwa jumuiya za kidini, kukomeshwa usimamizi wa Wakfu wa Jaafari, kukamatwa na kufukuzwa maulama wakubwa, na hatimaye kuidhalilisha dhima ya kisheria ya kutoa hotuba, kuongoza na kutoa mawaidha kwa kuifanya itegemee idhini ya awali kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani.

Utawala wa Al Khalifa unaendesha mpango wa wazi unaolenga uwepo wa Mashia nchini Bahrain. Muungano huo umewataka watu wote kueleza kwa usahihi kile kinachotokea ardhini na kukitambua kuwa ni mauaji ya kimbari ya wazi, ambayo lengo lake ni kuangamiza utambulisho wa raia wenye asili ya nchi hiyo, yaani Mashia. Pia umetaka kuchukuliwa mtazamo mpana wa kuandaa mpango kamili wa kukabiliana na hatari hii inayotishia uwepo wao, pamoja na kuweka msingi wa mjadala na hatua zitakazovuka hofu na dhana potofu ambazo Al Khalifa wenyewe wanazieneza miongoni mwa wananchi, kwa lengo la kuathiri fikra za umma, misimamo ya wasomi na nguvu za ndani.

Msimamo wa wananchi pamoja na viongozi wao wa kidini na kijamii ni kukataa maamuzi na hukumu zote zinazovamia utambulisho, imani na ibada zao, kutangaza kutotii dhidi yake na kutokubali kujisalimisha kwake; kwa sababu kujisalimisha mbele ya hukumu hizo kunapingana na fatwa ya kisheria, na kunarahisisha kazi ya utawala wa Al Khalifa katika kuwaangamiza wananchi wa Bahrain, huku kukiharakisha mchakato wa kuwageuza raia wenye asili ya nchi hiyo kuwa wachache wanaokandamizwa kwa idadi, kuwaangamiza na kuwasukuma kuelekea kwenye uharibifu, kutawanyika na kutoweka hatua kwa hatua. Hili ni jambo ambalo wananchi wanalikataa na hawataruhusu litimie, bali wataendelea kufuata njia ya mababu na baba zao katika kusimama na kupinga hadi kuwakomboa kutoka kwa wavamizi wa Al Khalifa.

Maadhimisho ya kusikitisha ya kutiwa saini makubaliano ya aibu na kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya utawala wa Kizayuni na utawala wa Al Khalifa yaliafikiws katikati ya mwezi Septemba. Makubaliano hayo yalikuwa mlango rasmi na wa wazi wa Al Khalifa kujiunga na muungano wa mauaji ya kimbari na uchokozi unaoongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran na dhidi ya mhimili wa Muqawama katika Ghaza, Ukingo wa Magharibi, Lebanon, Iraq na Yemen.

Msimamo wa wananchi wa Bahrain wa kukataa makubaliano ya kuhalalisha uhusiano na Israel pamoja na uwepo wa kituo cha kijasusi cha Kizayuni mjini Manama, ni sehemu ya msimamo wao wa kuunga mkono Muqawama na kukabiliana na nguvu za ubeberu. Ni msimamo ambao makubaliano ya Al Khalifa ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utegemezi, pamoja na sheria zao za ukandamizaji na unyanyasaji, hayawezi kuudhoofisha.

Baraza hilo limetahadharisha kwamba: “Firauni Hamad”, mfalme wa utawala wa Al Khalifa, anamalizia kipindi chake cha utawala kwa kuisukuma nchi kuelekea katika misukosuko mikubwa katika uthabiti wa kiuchumi na mamlaka ya kitaifa; kwani jumla ya deni la umma limefikia kiwango kisichokuwa na mfano cha dinari bilioni 20 za Bahrain. Hali hiyo inatokea sambamba na ufisadi wa kifedha uliopangwa kwa utaratibu, unaohusishwa na sera ya kugawana nyara baina ya “Salman”, mkuu wa serikali anayeendeleza uhusiano wa kawaida, na ndugu yake “Nasser”, ambaye anatajwa kuwa muuaji, kupitia udhibiti wao wa kampuni mbili za “Mumtalakat” na “Bapco Energies”. Jambo hili linaambatana na kuiunganisha nchi na sera za kigeni na kuifungamanisha na maslahi ya nguvu zenye kutawala na kufanya uchokozi, hali ambayo imesababisha kukiukwa kwa mamlaka ya Bahrain na kuhatarisha usalama wa wananchi pamoja na utulivu wa maisha yao, riziki zao na maisha yao yenye heshima.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha